SITTA: BUNGE MAALUM LA KATIBA KUENDELEA KAMA KAWAIDA

Friday, July 25, 2014

Na Winner Abraham na Rose Masaka-
MAELEZO-Dar es salaam

Mwenyekiti  wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa  Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama ulivyopangwa  Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.


Amesema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia  vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.


Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.


 “Kamati hiyo, imeamua  kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba  Bunge Maalum la Katiba liendelee   kwa  sababu  yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuikarabati Tume ya  Taifa ya Uchaguzi(NEC).


 “Mambo mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano,haki za wakulima,wafugaji,wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,”alisema Sitta katika taarifa hiyo.


 Aidha  aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa  zaidi ya theluthi  mbili   ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.


Alisema  hatua ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.


 Aliongeza kwamba Kamati hiyo, inaona  kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira halisi  ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji  kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.


 Alisema Kamati hiyo inarejea kwamba  wajumbe hao  629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.


“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.


 Mwenyekiti huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo,  uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye  inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu  zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.


 Alisema Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.


Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi,walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.


“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti  hadi  asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema  Sitta  katika taarifa yake. 


Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye  kuipigia kura Katiba mpya  ni pamoja na  kupoteza mabilioni ya fedha  za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno  mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.

RAIS KIKWETE AMWAPISHA LEO SHABAN ALLY KUWA JAJI KIONGOZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akimuapisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila leo jijini Dar es Salaam.
 Jaji Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jaji Shaban Ally Lila (kulia) akitia saini hati ya Kiapo mbele ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa hafla ya kuapishwa kwake  leo jijini Dar es Salaam. Katikati mwenye miwani Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akishuhudia tukio hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini hati ya Kiapo cha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila wakati wa hafla ya kuapishwa kwa jaji huyo leo jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi  hati ya Kiapo  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila wakati wa hafla ya kuapishwa kwa jaji huyo leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue(kushoto) akimpongeza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila mara baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo katika hafla iliyofanyika Ikulu leo jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahaka Kuu Tanzania mara baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo katika hafla iliyofanyika Ikulu leo jijini Dar es Salaam.Kushoto kwake ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman Picha zote na Frank Shija- MAELEZO

FUSO LAUA WAWILI NA KUJERUHI 46 SHINYANGA

-Walikuwa wanakwenda mnadani
-Wawili hali zao mahututi
Na Chibura Makorongo, Shinyanga
Watu wawili wamekufa papo hapo na wengine 46 kujeruhiwa baada ya lori aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria na mizigo yao kutoka katika kijiji cha Kiloleli kwenda katika mnada wa Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuacha njia na kupinduka kutokana na kile kilichotajwa kuwa mwendo kasi.

Ajali hiyo imetokea leo saa tatu asubuhi katika kijiji na kata ya Uchunga wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga baada ya lori lenye namba za usajili T680 ARL aina ya Fuso lililokuwa limepakiza mizigo na wafanyabiashara ambao idadi yao bado haijajulikana  likitokea kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu kwenda katika mnada wa Mhunze uliopo Kishapu liliacha njia na kupinduka.

Walioshuhudia ajali hiyo wamesema gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi likamshinda dereva, hivyo kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha amesema katika taarifa za awali zinaonyesha kuwa ajali hiyo imetokana na mwendo kasi wa lori hilo.

Amesema lori hilo aina ya Fuso, mali ya Ngasa Seni, mkazi wa Kiloleli lilikuwa likiendeshwa na Shija Ngasa ambaye pia ni mfanyabiashara, mkazi wa Kiloleli wilayani Kishapu ambaye alitoroka baada ya kutokea ajali hiyo na anatafutwa na jeshi la polisi.

“Lori hili lilikuwa linatoka Kiloleli kwenda Mhunze mnadani,lilikuwa limepakiza abiria wengi wakiwa wafanyabiashara,liliacha njia na kupinduka,chanzo mwendo kasi”,alifafanua kamanda Kamugisha.

“Taarifa za awali tulizonazo watu wawili wamefariki dunia,mmoja anaitwa Difa Shimo(28) mkazi wa Bulima Kishapu,mwingine jina lake bado halijafahamika,majeruhi wako 46, 35 wako katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga, 11 wapo katika Hospitali ya Kolandoto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga”,aliongeza Kamugisha.

Kufuatia ajali hiyo kamanda Kamugisha alitoa wito kwa wamiliki wa magari,wananchi wakiwemo wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia magari yasiyo ya abiria kusafiria.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dk. Maguja Daniel amesema wamepokea miili miwili ya marehemu na majeruhi 35 na wanaendelea kuwapatia matibabu huku wawili hali zao zikiwa mbaya.

Ajali hiyo ya Fuso imetokea ikiwa ni siku moja tu baada ya abiria 63 kunusurika kufa baada ya basi la Super najimunisa likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka katika eneo la kijiji cha Usanda kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

ELIMU DUNI NA ISIYO SAHIHI YA MATUMIZI YA KONDOMU INACHANGIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU KWA VIJANA

DSC_0084
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akizungumza na washauri wa Vikundi vya Vijana wasikilizaji juu ya masuala muhimu kuhusiana na kuzuia maambukizi ya VVU na Afya ya Uzazi kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 katika warsha ya kuwajengea uwezo washiriki hao katika matumizi ya mwongozo wa ufuatiliaji wa vipindi kwa wasikilizaji walengwa wa Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika kwenye kituo cha Redio Nuru FM mjini Iringa.(Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu
Tafiti zimebaini kwamba Vijana hawatumii Kondomu na hutoa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na kutopata ladha wakati wa tendo la ndoa na kwamba inapunguza nguvu na visingizio vingine vingi vinavyopelekea kuashiria hatari ya maambukizi.
Hayo yameelezwa na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias wakati akizungumza na washauri wa Vikundi vya Vijana wasikilizaji juu ya masuala muhimu kuhusiana na kuzuia maambukizi ya VVU na Afya ya Uzazi kwa Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 katika warsha ya kuwajengea uwezo washiriki hao katika matumizi ya mwongozo wa ufuatiliaji wa vipindi kwa wasikilizaji walengwa wa Mradi wa SHUGA Redio.
“Asilimia 40 ya Wasichana na Asilimia 47 ya Wavulana ndio wenye ufahamu wa kina juu ya maambukizi ya VVU huku asilimia kubwa wakiwa hawana elimu ya kutosha na hawajui afya zao kwa kuwa hawana utamaduni wa kupima VVU ”, amesema Bw. Mathias.
DSC_0184
Mkufunzi wa warsha hiyo Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akiwapiga msasa washauri wa Vikundi vya Vijana kwenye warsha ya siku mbili inayoendelea mjini Iringa.
Katika warsha hiyo ya siku mbili inayoendeshwa na UNESCO kwa kushirikiana na UNICEF katika kituo cha Redio cha Nuru FM Iringa, Bw. Mathias amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu sahihi kwa Vijana ya kujikinga na maambukizi ya VVU na Mimba kutokana na uelewa mdogo wa Vijana katika matumizi sahihi ya Kondomu.
Wakichangia mada kuhusu masuala muhimu yanayowahusu vijana katika maambukizi ya VVU vijana wamesikitishwa na mimba za utotoni kwa wasichana zinazochangia vifo vya Mama na Watoto na wasichana kuacha masomo.
Washiriki wa warsha hiyo wametaka hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha kuwa sheria za mtoto zinazoruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri mdogo zinafanyiwa marekebisho ya haraka kulinda haki ya mtoto wa kike.
DSC_0139
Mmoja wa washiriki akihoji jambo kwa mkufunzi wakati wa mafunzo hayo.
Wakijadili mada hiyo washiriki wamesema mila na tamaduni pia zinachangia kwa kiasi kikubwa kumkandamiza mtoto wa kike katika masuala mbalimbali ya maendeleo yake.
Wakitoa mifano ya baadhi ya mila zilizowafanya wapaze sauti kuhusu mabadiliko ya sheria za mtoto ni ile sheria ya ndoa na mila inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi. Umri huo unakinzana na haki za mtoto kufurahia maisha yake na kupata elimu.
Mifano mingine ya kitamaduni ni pale mwanamume anapochumbia mimba wakati akijua wazi mtoto ana haki zake za msingi za kuishi.
Wamezitaja pia asasi za dini kutoa elimu kwa vijana ili kusaidia hali iliyojitokeza ya wazazi kutokuwa na muda na watoto wao kuwaelimisha kuhusu mabadiliko ya miili na afya zao.
DSC_0089
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akifafanua jambo kwa washiriki.
Akitoa mada kuhusu mbinu mbalimbali za kuwezesha majadiliano katika vikundi vya wasikilizaji, Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdul Mfuruki amewataka wawezeshaji kutotumia nafasi walizonazo ili kuendesha mjadala wenye tija.
Amesema washauri wa vikundi hawana budi kuweka mizania kutumia busara, kusoma mazingira na kutoingiza imani au itikadi itakayopelekea kuharibu mjadala unaoendeshwa wa kufuatilia vipindi vya SHUGA Redio, kuwa wavumilivu, kusoma na kuheshimu mawazo ya wengine na kutofungamana na upande wowote ili kumweleza mshiriki wa majadiliano kufunguka zaidi.
Bw. Mfuruki amesema vijana wa vikundi vya wasikilizaji kuwaza mambo mengi ni vyema kuwasikiliza kwa uvumilivu, kupata ushauri wa wengi kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi bila kulazimishana na vile vile kuwa wabunifu kwa kutumia mbinu mbadala ili kupata habari iliyojificha.
DSC_0114
Mkufunzi Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akiwaelekeza jambo washiriki wakati wa mazoezi ya vikundi kazi kwenye warsha hiyo.
DSC_0075
Pichani juu na chini ni baadhi washauri wa vikundi vya vijana wakifuatilia kwa umakini warsha hiyo kwa ajili ya kutekeleza Mradi mpya wa SHUGA Redio wenye lengo la kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya VVU kupitia Redio za Jamii nchini.
DSC_0091
DSC_0120
Pichani juu na chini ni Washiriki wakijidiliana kwenye vikundi kazi wakati wa warsha hiyo.
DSC_0124
DSC_0182
Mkufunzi wa warsha hiyo Meneja Mawasiliano kutoka Pangani FM, Bw. Abdullah Mfuruki akitoa mwongozo wa kazi za vikundi kwa staili ya aina yake kwa washiriki wa warsha ya siku mbili katika utekelezaji wa Mradi mpya wa SHUGA Redio.
DSC_0203
Pichani juu na chini washiriki akitolea maelezo ya picha aliyoichora ikimaanisha nini wakati wa warsha hiyo ya siku mbili inayoendelea mjini Iringa.
DSC_0221

UGOMVI WA ISRAEL NA PALESTINA HADI KWENYE SOKA! WAANDAMANAJI WAVAMIA UWANJA NA KUZIPIGA

Thursday, July 24, 2014

Attack: Protestors storm the pitch and appear to attack the Maccabi Haifa players
Mashambulizi: Waandamanaji walivamia uwanja na kuanzisha dhoruba ya kuwashambulia wachezaji wa  Maccabi Haifa
Ugly scenes: Protestors attack the Maccabi Haifa players forcing the game to be called off early
Hatari sana: Waandamanaji waliwavamiwa wachezaji wa Maccabi Haifa na kusababisha mechi kuahirishwa.
Brawl: Protestors and Maccabi Haifa players clash after the game is stopped
Waandamanaji wakizipiga ngumi na wachezaji wa Maccabi Haifa 
Hitting back: Several Maccabi Haifa players were spotted fighting back after being attacked
Jamaa akaamua kumrudishia: Wachezaji wengi wa Maccabi Haifa walianza kuzipiga baada ya kuvamiwa
Tension: Pro-Palestinian supporters attacked the Maccabi Haifa players
Kula buti kwanza kijana!: Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina waliwavamiwa wachezaji wa  Maccabi Haifa

MECHI kati ya timu Israeli ya Maccabi dhidi ya Lille ya Ufaransa iliahirishwa baada ya waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina kuvamiwa uwanja.
Waandamanaji hao walioripotiwa kuwa na asili ya Uturuki waliingia katika uwanja wa Austrian ambapo mchezo ulikuwa unaendelea na kuwavamia wachezaji wa Maccabi na kuzua vurugu.
Mmoja wa wachezaji alionekana akizozana na shabiki kabla ya kuanza kurushiana makonde mazito. Hata hivyo wachezaji wa Maccabi walifanikiwa kutoka uwanjani bila kujeruhiwa.
Tukio hili limekuja wakati huu ambao majeshi ya Israel yamevamia na kufanya uhalifu dhidi ya majeshi ya Hamas huko Gaza

PINDA AFUNGUA MKUTANO WA BRN PIA AWASILI NAIROBI KUMWAKILISHA KIKWETE MKUTANO WA MAZIWA MAKUU

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiongozana na Katibu Mkuu, Kiongozi, Balozi Seif Sefue  (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Dr. Omari Issa baada ya kufungua mkutano wa Mawaziri na Makatibu Wakuu kuhusu BRN kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam Julai 24, 2014.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimana na Seneta wa Kirinyaga, Daniel Dickson Karaba baada ya kuwasili  wenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya  Julai 23, 2014 kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano maalum wa nchi za maziwa makuu kuhusu kupambana na tatizo la ajira kwa vijana unaotarajiwa kufanyiaka Julai 24, 2014.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimana na baadhi ya watumishi wa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya  baada ya kuwasili  wenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta   Julai 23, 2014 kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano maalum wa nchi za maziwa makuu kuhusu kupambana na tatizo la ajira kwa vijana unaotarajiwa kufanyiaka Julai 24, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

CRAWFORD SMITH FOUNDATION YAKUSUDIA KUSAMBAZA HUDUMA YA MAKTABA KWA WENGI

 Kutoka kushoto ni  Bw. Steven Smith,  Bi Ann Hanin, Mhe.  Balozi   Tuvako Manongi na Bibi Judith Smith


NA MWADISHI WETU, NEWYORK
Baada ya  kuridhishwa  na matumizi mazuri  na mafanikio makubwa ya    Maktaba yao ya kwanza waliyoifungua mwaka 2009 katika  kijiji cha Ngongongare   Mkoani Arusha.


Taasisis isiyo ya kiserikali ya  The Crawford Smith Foundation yenye   makazi yake  nchini Marekani na  ambayo ndiyo inayosimamia mradi wa  uanzishwa na uendeshaji wa Maktaba hususani katika maeneo ya   vijijini,   sasa inakusudia kujenga maktaba  nyingine sita katika maeneo mbalimbali  nchini Tanzania.

 Maktaba  hiyo ya kwanza na ya aina yake  na ambayo imepewa jina la  Jifundishe Free Library,   si tu inatoa huduma za vitabu vya kiada na ziada  kwa watumiaji  ambao ni kuanzia wale wa shule za awali, msingi, sekondari na hata vyuo vikuu, bali pia imekuwa kituo   ambacho  kinawasaidia wanawake na vijana   kujifunza  stadi mbalimbali zikiwamo za ujasiliamali,  vyama ya  kuweka na kukopa, huduma za  kinga ya afya, huduma za   internet na  mafunzo  ya ziada ambayo yamekuwa yakitolewa na wataalamu wa kujitolea kutoka nje na ndani ya  Tanzania.

Hayo yameelewa na Viongozi wakuu wa Taasisi hiyo ya  The Crasford Smith Foundation wakati  walipofika na kufanya Mazungumzo  na   Balozi Tuvako Manongi Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

 Kwa mujibu wa  maelezo ya Bw. Steven Smith aliyekuwa amefuatana na Mke wake  Bibi. Judithi Smith   amesema kuwa  mwitikio mkubwa  na matumizi sahihi na endelevu vya  Jifundishe  Free Library  na matokeo mazuri ya wanafunzi katika mitihani  yao,  kumewafanya  watambue ni kwa kiasi gani huduma hiyo  muhimu  inahitaji  kusambazwa  katika maeneo mengine hasa ya vijijini. Lengo  likiwa ni kuwafikia na kuwapatia huduma hiyo  wasio kuwa na uwezo wa kuipata kwa urahisi.

Mradi huo wa  Maktaba  licha ya kutoa huduma mbalimbali,  lakini umekwenda mbali zaidi kwa kutoa ufadhili  wa masomo  ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi  wanne hadi sasa. baadhi ya wanafunzi hao wamerudi na kutoa mchango wao  katika   Maktaba hiyo na jumuiya inayoizunguka.

Baadhi ya  maeneo ambako wanakusudia kupelea huduma hiyo muhimu ya maktaba ni  Kisarawe , Chunya , Iringa,  Morogoro na  Kilimanjaro.  Aidha wakuu hao wameeleza  kuridhidhwa kwao na  Ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Serikali  akiwamo  Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,  baadhi ya   Makampuni ambayo yameonyesha nia ya kushirikia na Taasisi hiyo katika  utoaji wa huduma hiyo, na vilevile mwamko na moyo  wakujitolea wa watanzania  katika maeneo wanayokusudia kuanzisha maktaba  hizo.


Kwa upande wake,  Mhe. Balozi   Balozi Manongi aliishukuru Taasisi hiyo kwa mchango wake mkubwa na ambao umeonyesha  mafanikio na mabadiliko makubwa kwa jamii inayohudumiwa. Akasema Tanzania inatambua umuhimu wa maktaba katika mustakabali mzima wa elimu na mafunzo na kwamba mchango wa taasisi zisizo za kiserikali unakaribishwa sana.